Wednesday, 7 December 2016

Ifikapo 2017 vituo vyote vya Tv viwe na wakalimani wa lugha ya alama

Katika kuadhimisha ya Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ameagiza vituo vyote vya runinga nchini ifikapo Machi mwaka 2017, kuweka wakalimani wa lugha za alama katika taarifa za habari na matukio ili watu wenye ulemavu wa kusikia wapate habari .
“Ifikapo 2017 vituo vyote vya Tv viwe na wakalimani wa lugha ya alama ili kutekeleza matakwa ya sheria namba 9 hasa katika habari ili walemavu wafuatilie matukio na habari bila ya kuachwa nyuma,” amesema.
Pia amewataka watendaji wa serikali kupanga mipango itakayojibu mahitaji ya watu wenye ulemavu nchini.
Pia ameagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuwasimamia waganga wakuu kuagiza mafuta ya kuzuia athari za mionzi ya jua kwa watu wenye ulemavu wa ngozi katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
“Natoa agizo kwa wakurugenzi wa halmashauri nchini wawasimamie waganga wakuu wanapoagiza dawa MSD waagize na mafuta ya kukinga mionzi ya jua dhidi ya ngozi za maalbino, ili kundi hilo lipate mafuta hayo kwa uraisi. MSD pia ijumuishe mafuta ya ngozi katika orodha ya dawa inazoagiza,” alisema.
Pia Mhagama amewaagiza watendaji wa serikali kuunda kamati za watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya kata ili ziratibu changamoto za walemavu kwa ajili ya serikali kutenga bajeti ya kutatua changamoto hizo.
“Watendaji wa serikali waunde kamati za watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya mtaa ili ziweze kujadili changamoto za watu wenye ulemavu. Kamati hizi ziundwe ili bajeti zake ziingie katika bajeti kuu ya serikali,” alisema.
Kuhusu walemavu kupewa msamaha wa matibabu, amesema wizara yake kwa kushirikiana na wizara ya afya inandaa utaratibu wa walemavu kupata huduma ya afya bure bila kubaguliwa.
“Tumekaa na wizara ya afya kuandaa taratibu za walemavu kupata huduma bila kubaguliwa, hivi karibuni changamoto yenu itakwisha,” alisema.
Aidha, amevitaka vyama vya watu wenye ulemavu nchini kuadhimisha siku ya walemavu duniani katika mikoa yote ili kuongeza uelewa kwa wananchi na walemavu kupatiwa stahiki zao.

No comments:

Featured Post

Ronaldo kaonyesha yeye ni mwamba dhidi ya Salah

Mchezaji  wa klabu ya Real Madrid na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno amefunga magoli mawili  (2) katika mechi kati ya Ureno na Misri...