LeBron James amekuwa mchezaji wa kipekee msimu huu. Wakati wengi wakiona kama mchezaji ambaye angeweza kupungua kasi kutokana na umri, Lebron ameendelea kuwa kinyume na matarajio ya wengi na badala yake anacheza katika kiwango ambacho ni inawezekana kikawa bora zaidi kwa msimu huu wote katika hatua hii ya mtoano.
Baada ya kucheza vyema dhidi ya vilabu vya Indiana Pacers na Toronto Raptors kwenye hatua ya kwanza na ile ya nusu fainali na kuwaondoa pasipo kupoteza, Lebron ameendelea kuwakera na kuwadhihaki wapinzani wanaomlinda akifanya kila kitu kionekane kuwa rahisi.
Dhidi ya Boston Celtics kwenye mchezo wa fainali wa kanda ya Mashariki, Lebron ameiongoza klabu yake ya Cleveland Cavaliers kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Boston Celtics kwa kuibuka na ushindi wa 117-104.
James alimaliza mchezo akiwa na pointi 38, akadaka rebound 9 na kutoa pasi 7. Kevin Love alikuwa na kiwango bora na kufunga pointi nyingi zaidi katika maisha yake ya hatua za mtoano akimaliza na alama 32 na kudaka rebound 12 na ikimaanisha kuwa Cavs sasa wameshinda michezo yote 9 ya hatua ya Mtoano. Msimu uliopita kabla ya kufika hatua ya Fainali ya NBA na kuutwaa ubingwa huo walianza hatua ya mtoano ya kanda ya Magharibi kwa 10-0.
Sasa inamaanisha kuwa Lebron James amefanikiwa kufunga walau pointi 35 katika michezo 5 mfululizo ya hatua ya mtoano inayoendelea. Kocha wa Cavaliers Tyronn Lue alisema ubora wa Lebron James unaendelea kufanya mambo kuwa rahisi kwa wachezaji wote katika pande zote za uwanja, yaani ulinzi na ushambuliaji.
Avery Bradley na Jae Crowder waliiongoza Celtics kwa kufunga pointi 21 kila mmoja huku mchezaji wao bora Isaiah Thomas akimaliza na pointi 17. Wakiwa wanatoka kushinda mchezo wao wa 7 wa nusu fainali dhidi ya Washington Wizards uliofanyika alfajiri ya Jumanne, Boston walikosa mitupo 11 kati ya 14.
No comments:
Post a Comment