Mshambuliaji wa kimataifa anayeitumikia klabu ya Dhofar SC ya nchini Oman, Elias Maguli amewataka vijana wa Kitanzania wanaotaka kuendeleza vipaji vyao, nje ya nchi kujaribu pale wanapopata nafasi na sio kukata tamaa.
Mshambuliaji wa kimataifa anayeitumikia klabu ya Dhofar SC ya nchini Oman, Elias Maguli.
Maguli amesema, vijana wengi wamekuwa wakipata nafasi za kwenda katika majaribio katika timu mbalimbali za nje ya nchi lakini wamekuwa wakikatishwa tamaa na baadhi ya watu wanaowazunguka .
"Kwanza wanapopata nafasi waende. Hawawezi kupata taarifa kwamba kuna ubaguzi katika hiyo nchi unayotakiwa kwenda kabla hujafika. Fika kwanza ndio ujue matatizo yaliyopo katika hiyo nchi, na mimi nina imani kuna wachezaji wengi wamepata nafasi lakini labda wao wanapenda kucheza hapa nchini,” amesema Elias Maguli.
Maguli ameongeza kwa kuvitaka vilabu vya soka hapa nchini kuwaruhusu wachezaji ili waweze kutumia nafasi wanazozipata nje ya nchi
“Kunawachezaji wengine wameshapata nafasi lakini vilabu vimekuwa tatizo, kwani vilabu mara nyingi huwa vinawakatalia wachezaji na hata kutaja dau kubwa na ukiangalia sisi wachezaji wa hapa Tanzania katika viwango bado tupo chini, hivyo tunapopata nafasi ni lazima kuzitumia ili kuweza kukuza zaidi vipaji vyetu, ” alisisitiza Maguli.
Maguli amewataka wachezaji kutokuogopa changamoto katika soka kwani changamoto wanazokutana nazo ndizo zinasaidia kuweza kuwakuza katika soka.
“Unajua Tanzania kukiwa na wachezaji wengi wa kimataifa ingekuwa ni faida kwani kila mchezaji anapoitwa katika timu ya Taifa tungefanya vizuri zaidi ya hapa kwani kila mchezaji anakuja na uwezo wake aliofundishwa kutoka katika klabu yake, na pia tunajifunza vitu vingi katika maisha ya Soka, na tusiogope changamoto kwani changamoto hata hapa nchini zipo na ndizo zinazotusaidia kukua kisoka. Sasa kwa nini tuogope kwenda nje, tunahitaji kuwa wengi wa kimataifa, ” amesema Maguli.
No comments:
Post a Comment