Mashabiki wa Gor Mahia wanatarajia kutua nchini na kupata mapokezi kutoka kwa mashabiki wa Yanga.
Mashabiki wa Gor Mahia kutoka Kenya wanakuja Tanzania kushuhudia fainali ya SportPesa Super Cup wakati watakapocheza dhidi ya AFC Leopards kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Wakali hao wanakutana Jumapili katika mechi inayojulikana kama “Derby ya Mashemeji” na Gor Mahia wanaamini Yanga ndiyo rafiki zao.
Hii inatokana na aina ya ushabiki wa hizo timu na pia rangi kwa kuwa Yanga wanatumia rangi tatu ambazo ni kijani, njano na nyeusi wakati Gor Mahia ni kijani na nyeupe.
“Kweli kuna mashabiki wanakuja kutoka Kenya, wameondoka leo asubuhi. Ni wengi sana wanaweza kufika zaidi ya elfu tano na wanakuja kwa ajili ya mechi,” alisema Thomas Omond ambaye ni shabiki wa Gor Mahia na yuko jijini Dar es Salaam tokea kuanza kwa michuano ya SportPesa Super Cup.
“Sisi tunaona tunaendana na Yanga sana, hata ukiangalia rangi zetu tunafanana. Pia watu wa Yanga wameonyesha wako tayari kutupokea.
“Sasa tutaungana nao kushangilia siku hiyo kwa kuwa tunataka kuchukua ubingwa,” alisema Omond.
No comments:
Post a Comment