Mkuranga. Watu sita wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa baada ya basi mali ya kampuni ya Ibra Line walilokua wanasafiria kugongana uso kwa uso na basi lingine dogo katika barabara kuu ya Dar salaam - Kilwa.
Ajali hiyo imetokea jana jioni katika kijiji cha Njopeka, Tarafa ya Mkamba wilayani Mkuranga Mkoani Pwani.
Magari yaliyohusika na ajali hiyo ni basi aina ya Yutong mali ya kampuni ya Ibra Line lililokuwa linatokea Dar esalaam kwenda Masasi na gari Nissan Carava Hiace iliyokua ikitokea Jaribu Mpakani kwenda Dar esalaam.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Jafar Mohamed amethibitisha kutokea ajali hiyo na kusema imesababishwa na mwendo kasi wa basi na pia dereva wake alikua anayapita magari mengine bila tahadhari.
Amewataja abiria waliopoteza maisha katika tukio hilo ni Nasra Omary(13),Zainab Abdala (28), Hauma Abdala (35), Musa Matibwa (50) na mwingine ni mwanaume ambaye jina lake halikuweza kutambulika
Kamanda huyo wa Polisi Pwani ameongeza kuwa majeruhi wanne wa ajali hiyo wote walipelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi na kwamba majina yao hayakuweza kupatikana mara moja kutokana na hali zao kuwa mbaya.
Ameongeza kuwa tayari dereva wa basi hilo la Ibra Line lililohusika na ajali hiyo ameshakamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakani wakati wowote kuanzia sasa.
No comments:
Post a Comment