Friday, 27 November 2015

Marehemu Alphonce Mawazo Kuagwa na Kuzikwa

CHADEMA Yashinda Kesi......Mahakama Yatoa Kibali Mwili wa Marehemu Alphonce Mawazo Kuagwa na Kuzikwa


Mahakama kuu kanda ya Mwanza imetoa hukumu ya kuondoa zuio la kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza la kuinyima familia ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kibali cha kuuaga mwili wa marehemu Alphonce Mawazo katika jiji la Mwanza.

Hukumu ya kesi hiyo iliyovuta umati mkubwa wa wakazi wa jiji la Mwanza na mikoa jirani ya kanda ya ziwa, imetolewa leo mchana na jaji Lameck Mlacha, baada ya familia ya marehemu kupitia kwa baba yake mdogo mchungaji Charles Lugiko kufungua kesi ya madai dhidi ya kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza na mwanasheria mkuu wa serikali ya kupinga marufuku ya jeshi la polisi mkoani humo kuaga mwili wa Alphonce Mawazo kwa madai kwamba jijini Mwanza kuna mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu na taarifa zao za kiitelejensia zilibaini kwamba kungetokea uvunjifu wa amani.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua muda wa saa moja na dakika 33, Mhe. Jaji Lameck Mlacha amesema kuwa baada ya kupitia maombi ya mapitio ya Charles Lugiko dhidi ya kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza chini ya hati ya dharura, ameona kuna utofauti mkubwa katika zuio hilo na kusema kuwa marehemu ana haki zote za kuagwa na ndugu, jamaa, marafiki na wafuasi wa chama chake na pia anayo haki ya kufanyiwa taratibu za ibada, huku akiongeza kwamba mtu asiangaliwe kwa historia yake ya nyuma bali aangaliwe sasa.

Amesema kama kamanda wa polisi alikuwa na taarifa za kiitelenjesia hakuwa na sababu ya kuweka katazo, bali alitakiwa kuwaita ndugu na viongozi wa CHADEMA na kuzungumza nao kwa ajili ya kujitetea na wala si kuwanyima haki yao ya kikatiba, kwani haki ya kisheria ilikuwa ni kuwaita wote.

Baada ya kutoa hukumu hiyo, Jaji Lameck alitoa maelekezo ya kuzingatiwa na pande zote mbili, ambapo amesema mtoa maombi ambaye ni baba mdogo wa marehemu Alphonce Mawazo, mjibu maombi wa kwanza – kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza na viongozi wa CHADEMA wakutane haraka kwa ajili ya kuweka taratibu za ibada na kuaga mwili.

No comments:

Featured Post

Ronaldo kaonyesha yeye ni mwamba dhidi ya Salah

Mchezaji  wa klabu ya Real Madrid na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno amefunga magoli mawili  (2) katika mechi kati ya Ureno na Misri...