Uyoga
ni zao la viumbe hai viitwavyo kuvu (fungi). Tanzania inao utajiri
mkubwa wa uyoga wa asili. Uyoga wetu wa asili hupatikana wakati wa msimu
wa mvua tu. Hili ni tatizo kubwa kwa vile wananchi walio wengi hupenda
kula uyoga wakati wote.
Kwa
sababu ya upatikanaji wa uyoga kwa msimu, na kwa vile aina nyingine za
uyoga wa kienyeji zina sumu, tumefanya jitihada za kuanzisha kilimo cha
uyoga ili kukidhi mahitaji ya wananchi kwa mwaka mzima. Pamoja na kutoa
lishe bora kwa watu, uyoga pia unaweza kuzalishwa kama zao la biashara.
UMUHIMU WA ZAO LA UYOGA.
Uyoga kama chakula una
viinilishe vingi vilivyo muhimu kwa afya ya binadamu. Uyoga una protini
kati ya 3-4. Pia una vitamini B, C, D na K. Uyoga pia una madini
yanayohitajika katika mwili wa binadamu.
Uyoga ukitumika kama
sehemu ya chakula cha familia mara kwa mara hutibu au kuzuia magonjwa
kama vile saratani, vidonda vya tumbo, shinikizo la damu pia huongeza
kinga ya mwili.
Kilimo cha uyoga
huchangia pato la kaya na hutoa ajira. Kilimo hiki ni kizuri kwa wazee,
akina mama na vijana kwa vile hakihitaji mtaji mkubwa kuanzisha na
mavuno hupatikana baada ya muda mfupi. Aidha kilimo hiki hakihitaji eneo
kubwa kama mawazo mengine kwani uyoga huoteshwa ndani ya banda.
MAHITAJI YA KUANZISHA KILIMO CHA UYOGA.
1. Mbegu
Kama mazao mengine; ili
kuanzisha kilimo cha uyoga unahitaji mbegu. Maabara za mbegu za uyoga
ziko Uyole hutoa aina mbalimbali za uyoga kwa bei ya nafuu.
2. Masalia ya mazao ya kilimo.
Kilimo cha uyoga hutumia
masalia ya mazao ya kilimo kwa mfano majani ya mpunga, maharage,
migomba, magunzi, mabua na ngano. Kwa ujumla kilimo cha uyoga hutunza
mazingira kwa vile uchomaji wa masalia ya mazao ya kilimo huharibu
mazingira.
Mabaki ya kilimo uyoga yanaweza kutumika kama mbolea, chakula cha mifugo au kuzalisha nishati ya gesi.
3. Banda.
Uyoga hulimwa ndani ya
banda. Banda ligawanywe katika vyumba viwili, chumba chenye giza na
chumba chenye mwanga na hewa. Banda liezekwe kwa nyasi (bati huleta
tofauti ya joto kati ya mchana na usiku).
4. Kichanja au meza.
Kwa ajili ya kupozea majani na vifaa vya kupandia uyoga.
5. Pipa au sufuria kubwa.
Kwa ajili ya kuchemsha ili kuua wadudu na vimelea vya magonjwa kwenye masalia ya mazao ya kilimo.
6. Mifuko ya plastiki na kamba.
Uyoga hupandwa kwenye mifuko ya plastiki ambayo baada ya kupandwa hufungwa kwa kamba.
7. Hatua za kilimo cha uyoga.
- Fanya usafi kwenye banda la kulimia uyoga.
- Chambua masalia ya mazao ya kilimo (ondoa yenye rangi ya kijani) kisha osha kuondoa vumbi na uchafu mwingine.
- Weka maji theluthi moja ya chombo cha kufukizia.
- Jaza vimeng'enywa kwenye pipa, funika na fukiza angalau kwa saa mbili (tangu mvuke unavyotokea juu ya mfuniko).
- Ipua kwenye kichanja au meza iliyooshwa.
- Ikisha poa , angalia
unyevu uliobaki kwenye vimeng'enywa kwa kukamua vimeng'enywa. Kama
matone ya maji yanatoka; anza kupanda. Kama maji yanachuruzika bado kwa
hiyo endelea kusambaza ili maji yatoke.
- Baada ya kunawa, sia
kwenye mfuko wa plastiki tabaka ya vimeng'enywa ikifuatiwa na mbegu
mpaka mfuko umejaa. Mwishoni weka tabaka la mbegu kisha funga mfuko kwa
kamba.
- Toboa mashimo kama 8 kupitisha hewa juu, katikati na chini ya mfuko; kwa kutumia uma au kijiko.
- Weka mifuko kwenye
chumba chenye giza ili mbegu ziote na utandu ufunike mfuko wote . Hii
itachukua wiki 2-3 kutegemea na hali ya hewa.
- Hamisha mifuko kwenye chumba chenye mwanga na hewa ili uyoga uote.
- Uyoga utaota baada ya
siku 7 mpaka 10. Vuna baada ya siku 4. Endelea kuvuna mpaka mavuno
yatakapofifia (baada ya miezi miwili hivi).
Imeandaliwa: Buberwa Robert
No comments:
Post a Comment