Vinara wa ligi ya Vodacom Simba kesho wanaondoka kuelekea mkoani Kagera kwa ajili ya pambano lao dhidi ya Kagera Sugar na baadaye wataelekea Mwanza kwa ajili ya kucheza na Mbao FC na Toto Afrcans.
Kocha Joseph Omog, amewajumuisha wachezaji 20, lakini amemwacha beki tegemezi Method Mwanjali kutokana na matatizo ya goti ambayo bado yanamsumbua.
“Nalazimika kumwacha Mwanjali, sababu bado anasumbuliwa na goti na tunakwenda mapema lengo likiwa ni kuzoea mazingira na kupata ushindi katika mechi zetu tatu tutakazocheza huko,”amesema Omog.
Kocha huyo amesema wanatambua kuwa michezo hiyo ni migumu ndiyo maana wanakwenda na tahadhari kubwa lengo ni kuhakikisha wanacheza kwa nguvu na kushinda mechi hizo ili kupata ubingwa.
Omog raia wa Cameroon amesema anajua uwezo wa timu zote tatu wanazokwenda kucheza nazo hivyo wamejipanga kuhakikisha wanacheza kwa umakini na kupata matokeo yatakayowapa ubingwa msimu huu.
“Ninaimani na wachezaji wangu kila mmoja kati yao ana ari ya kutaka mafanikio na kipindi hiki ndiyo muhimu kwao kuhakikisha wanacheza kwa nguvu na kupata kile wanachohitaji kwasasa,” amesema Omog.
Kocha huyo amewataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwaombea dua ili waweze kufanya vizuri kwenye mechi hizo ambazo ndizo zilizoshikilia ubingwa wao msimu huu
No comments:
Post a Comment