klabu ya Yanga yatoa sare na Klabu ya Zanaco uwanja wa Taifa
Mabingwa wa Tanzania, Yanga SC imejipa mtihani mgumu katika mchezo wa marudiano wa michuano ya klabu bingwa Afrika baada ya leo kulazimishwa sare na Zanaco kutoka Zambia katika dimba la Taifa Dar es Salaam.
Mchezo huo wa kwanza wa raundi ya kwanza umeshuhudia Yanga ikianza bila matumaini kwa kudhibitiwa kikamilifu katika dakika 20 za kwanza huku ikishambuliwa zaidi, na kama Zanaco wangekuwa makini wangeweza kuandika bao la mapema.
Baada ya dakika hizo, Yanga ilionekana kuimarika zaidi kwa kufanya mashambulizi kadhaa na hatimaye kupata bao safi kupitia kwa Saimon Msuva aliyefanya kazi nzuri akipokea pasi ya kitaalam kutoka kwa mkata umeme Justine Zullu ikiwa ni dakika ya 39.
Kipindi cha pili Yanga waliingia wakiwa wameongeza nguvu, lakini wakashindwa kutumia nafasi kadhaa walizopata, lakini waligeuziwa kibao katika dakika 20 za mwisho ambapo walishambuliwa mfululizo, na hatimaye Zanaco kupata bao la kusawazisha katika dakika ya 78 kupitia kwa Kwame na kufanya mchezo umalizike kwa sare ya bao 1-1.
Saimon Msuva - Mfungaji wa bao la Yanga
Mara baada ya mchezo nahodha wa Yanga Nadir Haroub amesema wameyapokea matokeo kwa kuwa ndivyo mchezo ulivyo, lakini watajipanga kwa ajili ya ushindi katika mchezo wa marudio, huku Zanaco wakionekana kumkubali zaidi Saimon Msuva na kumtaja kuwa ndiye nguzo ya Yaga kwa sasa pamoja na kuonekana kuridhika na matokeo.
Kwa matokeo hayo, Yanga italazimika kushinda katika mchezo wa marudiano, au kupata sare ya kuanzia mabao 2-2 na kuendelea.
No comments:
Post a Comment