“NILIANZA kucheza soka la mtaani, lakini baadaye kuna kocha Mzungu alikuwa anainoa Majimaji, anaitwa Samsolov, aliniona na kutaka kunipeleka Ulaya kuniendeleza kisoka, alipoenda kwa wazazi wangu baba akakataa, lakini yule Mzungu akawaambia Majimaji kwamba wanilee vizuri kwani ni hazina kubwa nitakuja kuwasaidia hapo baadaye,” anaanza kusimulia nyota wa zamani wa Taifa Stars na Simba, Steven Mapunda ‘Garincha’.
Garincha atakumbukwa zaidi na Wanasimba kutokana na kukabidhiwa unahodha na kufanikisha kuwaondosha waliokuwa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Zamalek, mwaka 2003.
Anasema katika maisha yake ya soka, amefanikiwa kucheza timu mbili tu za klabu zilizoshiriki Ligi Kuu Bara. Timu hizo ni Simba na Majimaji, alianzia Majimaji kabla ya kuhamia Simba.
“Nimezaliwa mwaka 1975 katika Kijiji cha Luwanda kilichopo Wilaya ya Mbinga mkoani Songea, nimekulia na kusoma hukohuko.
“Baadaye nikiwa na wazazi wangu, tukahamia Songea Mjini ambapo mpaka sasa nipo hapo na familia yangu kwani nimejenga.
Baba kuzuia kuondoka na Mzungu
“Sasa baada ya yule Mzungu ombi lake kufeli kutokana na baba yangu kukataa mimi kuondoka naye, Majimaji kweli walinilea na baadaye nikaja kuwa mchezaji wao kuanzia mwaka 1997 mpaka 1999.
“Kabla sijajiunga na Majimaji, niliwahi kucheza Tigger ya Mbeya, ilikuwa ikishiriki ligi za madaraja ya chini. Nilipokuwa Majimaji, niliisaidia kuchukua ubingwa wa ligi kuu msimu wa mwaka 1998.
“Kikubwa ninachoweza kusema ni kwamba, nikiwa Majimaji, mafanikio makubwa niliyoyapata ni kuchukua ubingwa huo wa ligi, lakini pia kwa miaka yote tulikuwa tukicheza Kombe la Muungano ambalo lilikuwa likihusisha timu sita, tatu za Tanzania Bara na tatu kutoka Zanzibar.
“Kwa tafsiri ya harakaharaka ni kwamba, kwa muda wote niliokaa Majimaji, hatukuwahi kutoka ndani ya tatu bora ndiyo maana tulikuwa tukishiriki michuano hiyo ambayo huchukua timu tatu za juu kutoka ligi ya Bara na ile ya Zanzibar.
“Baada ya kucheza kwa kiwango kikubwa ndani ya Majimaji, mwishoni mwa mwaka 1999, nikafanikiwa kujiunga na Simba.
“Aliyefanikisha mpaka mimi kujiunga na Simba ni mfanyabiashara, Mohammed Dewji ‘Mo’ kwani alikuwa anavutiwa sana na kiwango changu.
“Kabla ya hapo, Yanga waliwahi kunifuata kama mara mbili hivi, lakini walishindwa kuniondoa kutokana na kukutana na vikwazo mbalimbali kwa watu ambao hawakuwa tayari kuniona naondoka Majimaji.
“Simba nilicheza mpaka mwaka 2006 nilipoamua kurudi nyumbani Majimaji.
“Nikiwa Simba, tukio ambalo nalikumbuka mpaka leo ni kitendo cha sisi kuwaondoa Zamalek ya Misri waliokuwa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tuliwaondoa mwaka 2003 na kutinga robo fainali ya michuano hiyo bila ya wengi kutarajia. Wakati huo mimi nilikuwa nahodha.
Anatukumbusha kidogo ilivyokuwa
“Kwanza kabisa nikutajie baadhi ya wachezaji waliokuwa kwenye kikosi cha kwanza. Alikuwepo Selemani Matola, Boniphace Pawasa, Juma Kaseja na Ramadhan Waso.
“Nakumbuka maandalizi ya mechi hiyo hayakuwa ya kutisha sana, lakini naweza kusema jukumu nililopewa kwa kiasi kikubwa lilichangia tukasonga mbele.
“Ilikuwa hivi, baada ya kwenda Zambia kucheza dhidi ya Nkana, kuna wachezaji wetu watano wa kikosi cha kwanza walikuwa wamefungiwa wasicheze mechi ya marudiano, hivyo Kocha Aggrey Siang’a akanipa jukumu la kuwaongoza wenzangu. Yaani nikapewa unahodha.
“Kwanza nilimwambia kocha kuwa mimi siwezi majukumu hayo, alipoona naendelea kumkatalia ombi lake, akaamua kuwaita wazee waweze kuniweka chini ili nikubali, mwisho wa siku nikakubali.
“Mechi ya marudiano, tuliwafunga 3-0, ilipigwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Ikafuata mechi dhidi ya BDF XI ya Botswana. Hapa nyumbani tukawafunga bao 1-0, bao hilo nililifunga mimi.
“Kutokana na ushindi huo kuonekana ni mdogo, Watanzania wakaona ndiyo mwisho wa safari yetu, hakuna aliyetupa nafasi ya kusonga mbele.
“Cha kushangaza ni kwamba, tulipoenda kwao tukawafunga 3-1, tukasonga mbele. Tukacheza na Santos ya Afrika Kusini, mechi zote zikawa 0-0, tukasonga mbele kwa penalti 9-8. Ilipomalizika mechi hiyo, mechi iliyofuata ndiyo ilikuwa dhidi ya Zamalek.
“Kabla ya mechi hiyo nakumbuka alikuja Waziri Mkuu Frederick Sumaye, tukafanya kikao Uwanja wa Taifa ambao sasa unaitwa Uwanja wa Uhuru.
“Majadiliano yakaanza kufanyika kwamba tufanye nini ili tuweze kuwaondosha Zamalek kwani mara kadhaa timu za Waarabu zimekuwa zikizisumbua sana timu za Tanzania na kuzitoa kila zinapokutana.
“Wakati majadiliano yakiendelea, wazee wa klabu wakanisimamisha ili niweze kuzungumza kwa niaba ya wenzangu.
“Binafsi nakumbuka miongoni mwa maneno niliyomwambia waziri ni kwamba tunatakiwa kufanya mambo ambayo yatatufanya tusonge mbele bila ya wasiwasi, ikitokea tumeshindwa labda bahati mbaya.
“Nilimwambia kwanza sisi ni masikini na wapinzani wetu huwa wanatumia sana udhaifu huo kutufunga kila tunapokutana nao.
“Kutokana na umasikini wetu, tunapoenda kwao hutugharamia kwa kila kitu, katika kufanya hivyo, kuna mambo huyafanya ya kiujanjaujanja, wanatufunga kirahisi.
“Sasa nikamwambia haya mambo yote sijui ya kutafuta hoteli ya kufikia tufanye wenyewe, nikasema kama hatuna uwezo huo basi tupo radhi kufikia hata ubalozini, tutalala kwenye magodoro. Tukamaliza kikao kwa makubaliano kwamba mambo yote tutafanya wenyewe.
Wiki ijayo Mapunda atazungumzia kuhusu zawadi aliyowahi kupewa na Mo, anayo mpaka leo, pia atafunguka kuhusu mamilioni ya Sokabet yatakavyoinufaisha Majimaji.
CHANZO: CHAMPIONI
No comments:
Post a Comment