Friday, 8 September 2017

United waweka Historia kwa Jezi ya Mchezaji wao Keane



Na Saleh Ally

MEI 5, 1999 Manchester ilijiweka katika nafasi nzuri ya kubeba kombe la tatu katika msimu mmoja. Mwaka huo ni maarufu sana kwa Klabu ya Manch-ester United chini ya uongozi wa Kocha Sir Alex Ferguson.

Manchester ilichukua makombe matatu kuanzia Kombe la FA, Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya, kama unakumbuka kwa mabao ya dakika za nyongeza kupitia kwa Teddy Sheringham na Ole Gunnar Solksjaer.

Manchester United ndiyo klabu kubwa zaidi kwa England na tatu maarufu zaidi duniani kote unapozungumzia mchezo wa mpira wa miguu.Muonekano wa jezi ya Roy Keane baada ya mvutano na mchezaji wa Liverpool mwaka 1999.[/capti on]
Mafanikio yake hadi ilipo sasa yana mengi ambako imepita na mabadiliko makubwa yalipatikana wakati wa kipindi cha Ferguson ambaye alijiunga nayo mwaka 1986 akitokea Aberdeen ya kwao Scotland.

Championi limekuwa gazeti la kwanza la michezo nchini, kufanya ziara ya kina ya mafunzo katika Klabu ya Manchester United na moja ya vitu vilivyokuwa na mvuto ni namna vifaa vinavyowekwa kama kumbukumbu kutokana na matukio.

Jezi aliyovaa Keane katika mechi dhidi ya Liverpool hiyo mwaka 1999, hadi leo iko katika sehemu ya makumbusho ya Klabu ya Manchester United na watu wamekuwa wakiingia kwa kiingilio kwenda kuishuhudia jezi hiyo pamoja na vifaa vingine mbalimbali.

Jezi ya Keane ilichanwa katika patashika ya mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2, bao la kusawazisha la Liverpool likiwa limefungwa na Paul Ince ambaye zamani alikuwa nyota wa Manchester United. Liverpool haikuwa na nafasi ya kubeba ubingwa, ilikuwa katika nafasi ya saba lakini ilitaka kuhakikisha inaharibu mambo.

Kama Manchester United ingepoteza, safari ingewakuta na Arsenal kuwa na nafasi ya kuwa bingwa. Sare hiyo kwa kuwa walikuwa na kiporo, baadaye iliwawezesha kuwa mabingwa.

Pamoja na jezi hiyo, viatu vya Sheringham aliyefunga bao katika dakika ya kwanza ya nyongeza na Solkjaer aliyefunga bao la pili katika dakika ya tatu ya nyongeza na kuipa Manchester United ubingwa wa Ulaya mbele ya Bayern Munich iliyokuwa imetangulia kufunga bao katika dakika ya 6 kupitia kwa Mario Basler, navyo vimehifadhiwa.

Ni viatu muhimu kwa historia ya Manchester United kuiwezesha kufika hapo ilipo na kuifanya kuwa moja ya klabu kubwa zaidi duniani katika michezo.

Viatu vingine ni vya Dwight Yorke. Alijulikana kama Smile Killer, yaani muuaji anayetabasamu, hii ilitokana na muonekano wake, muda wote alikuwa ni kama mtu anayetabasamu. Alifunga zaidi ya mabao 25 msimu huo na kuwa kiongozi wa mabao wakati Man United ikibeba makombe hayo matatu.

Kingine kinachoshangaza, hata jezi ya Eric Djemba-Djemba, raia wa Cameroon, ambaye Ferguson alimsajili kutoka Nantes ya Ufaransa akitaka achukue nafasi ya Keane. Alifanikiwa kucheza mechi 20 tu katika miaka mitatu ya Man United na mwisho ikaonekana amechemsha kweli.

Djemba-Djemba alikuwa gumzo kutokana na kufeli. Nikajiuliza vipi Man United wanaweka jezi ya mtu aliyefeli, lakini wao wanaamini tofauti kabisa, kwamba Djemba-Djemba ni sehemu ya mafanikio yao. Walipofeli, hawakurudia kosa tena na marekebisho yalipitia kwa kiungo huyo ambaye wameihifadhi jezi yake ya timu ya taifa ya Cameroon ndani ya jumba hilo la makumbusho.

Kinachovutia hapa, utaona Manchester United inaweka juu heshima ya wachezaji wake wa zamani kwa kuwa wanah-usika na mafa-nikio yaliyopo sasa.
Kinach-ovutia zaidi, kupitia heshima inayojenga kwa wachezaji wake, uhifadhi bora wa kumbukumbu, klabu hiyo inaendelea kuingiza fedha zaidi kwa kuwa watu hulipa pauni 12 (Sh 35,640), kutembelea tu ndani ya makumbusho hayo.
Maana yake, wana uhakika wa kuingiza mamilioni ya fedha ndani ya wiki moja, hivyo kuwa wamefaidika maradufu kuonyesha heshima au thamani ya wachezaji wao waliopita lakini kupitia wao sasa wanaingiza fedha na kuendelea kuitangaza klabu yao kwa kiwango cha juu kabisa.

Ukiwauliza Simba vilipo viatu vya Abdallah Kibadeni ‘Mputa’ wakati akifunga hat trick dhidi ya Yanga ambayo ni hat trick pekee ya mechi ya watani wa jadi, hakika hawawezi kukueleza chochote kama ambavyo ukiwauliza wakuonyeshe viatu vya Zamoyoni Mogela, Malota Soma, John Makelele na wengine.

No comments:

Featured Post

Ronaldo kaonyesha yeye ni mwamba dhidi ya Salah

Mchezaji  wa klabu ya Real Madrid na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno amefunga magoli mawili  (2) katika mechi kati ya Ureno na Misri...