Mamia wafariki katika mkanyagano Saudi
Arabia
Watu 717 waliokuwa wakishiriki sherehe za hija
wamefariki kwenye mkanyagano uliotokea karibu
na mji wa Mecca, maafisa nchini Saudi Arabia
wamesema.
Idara ya ulinzi wa raia nchini humo imesema
watu wengine 863 wamejeruhiwa katika kisa
hicho kilichotokea eneo la Mina, takriban kilomita
tano kutoka mji wa Mecca.
Maafa hayo yalitokea mahujaji takriban milioni
mbili walipokuwa wakishiriki moja ya kaida
muhimu za mwisho katika ibada za hija.
Ndio mkasa mbaya zaidi kutokea wakati wa hija
katika kipindi cha miaka 25.
Mahujaji husafiri hadi Mina wakati wa kuhiji
kurusha mawe saba kwenye nguzo saba
zijulikanazo kama Jamarat, ambazo huwakilisha
shetani.
Nguzo hizo zimo katika eneo ambalo inaaminika
Nabii Ibrahim alijaribiwa na shetani.
Watu walikuwa wakielekea eneo la kurushia
mawe, na wengine wakitokea huko pale ghafla
watu walipoanza kuanguka.
Kulikuwa na raia wa Nigeria, Niger, Chad na
Senegal miongoni mwa mataifa mengine.
Idara ya ulinzi wa raia Saudi Arabia imesema
mkanyagano huo ulitokea pale kulipotokea
"ongezeko la ghafla" la watu waliokuwa
wakielekea kwenye kwenye nguzo za kurushiwa
mawe.
Waziri wa afya wa Saudi Arabia Khaled al-Falih
amesema mkanyagano huo ulitokea kwa sababu
mahujaji walikosa kufuata maagizo.
"Wengi wa wahamiaji huenda bila kufuata ratiba
iliyowekwa," amesema.
Mwandishi wa BBC Hausa Tchima Illa Issoufou
aliyekuwa ameenda kuhiji ni mmoja wa
walioathirika. Anasema shangazi yake alifariki na
baadhi ya watu alioandamana nao hawajulikani
waliko.
"Watu walikuwa tu wakiimba jina la Allah, huku
wengine wakilia, wakiwemo watoto. Watu
walianguka sakafuni na hakukuwa na wa
kuwasaidia. Ni kana kwamba kila mtu alikuwa
anajijali mwenyewe," amesema.
Mkanyagano huo umetokea siku ya kwanza ya
sherehe za Eid al-Adha.
Idara ya ulinzi wa raia Saudi Arabia imesema
maafisa 4,000 wametumwa eneo hilo kusaidia
pamoja na wahudumu 200 wa huduma za
dharura.
Maandalizi ya ibada hizo za hija yalikuwa
yamekumbwa na mkasa baada ya kreni kuanguka
katika msikiti mkuu wa Mecca mwezi huu na
kuua watu 109.
Hii si mara ya kwanza kwa mikasa kutokea
wakati wa hija.
Mikasa mingine iliyotokea wakati wa kuhiji:
2006: Mahujaji 364 walifariki wakati wa kurushia
mawe mnara unaoashiria shetani
1997: Mahujaji 343 walifariki na 1,500 kujeruhiwa
kwenye mkasa wa moto
1994: 270 waliuawa katika mkanyagano
1990: Mahujaji 1,426 waliuawa katika
mkanyagano njia za kupitia chini za kuelekea
maeneo matakatifu
1987: Watu 400 walifariki maafisa wa serikali
walipokabiliana na waandamanaji waliounga
mkono Iran
No comments:
Post a Comment