Friday, 16 October 2015

Ndiyo, nitaifanya Z’bar kuwa Singapore, na sitanii” – Maalim Seif

“Ndiyo, nitaifanya Z’bar kuwa Singapore, na sitanii” – Maalim Seif

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, anakusudia kuuzindua rasmi mpango wake wa kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki mwishoni mwa wiki hii.
SingaporeAlisema anapozungumzia mpango huo huwa hafanyi utani bali anazungumza akiwa na mikakati maalum ya kuweza kuibadilisha Zanzibar kufikia lengo hilo.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ametoa kauli hiyo wakati akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika viwanja vya Mkwajuni, mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema tayari chama hicho kimeshapanga mikakati imara ya kuweza kuikomboa Zanzibar kiuchumi katika kipindi kifupi kijacho iwapo atachaguliwa kuiongoza Zanzibar.
Akizungumzia mafanikio ya safari yake ya kichama nchini Afrika ya Kusini, alisema alikutana na viongozi wa makampuni mbalimbali ya nchi hiyo ambao walikubali kushirikiana nae kuikomboa Zanzibar kiuchumi iwapo atachaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi mkuu ujao.
Kuhusu matarajio ya ushindi kwa chama hicho Maalim Seif amesema kina matarajio makubwa ya kupata ushindi na kuapa kuwa hakuna atakayeweza kuzuia mabadiliko hayo.
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wafuasi wa chama hicho katika viwanja vya jimbo la Mkwajuni.
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wafuasi wa chama hicho katika viwanja vya jimbo la Mkwajuni.
Alisema wananchi wa Zanzibar wameshajiika kuleta mabadiliko na kuwahimiza kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuweza kufikia malengo hayo.
Aliishauri Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kujiandaa kutoa matokeo ya uchaguzi mapema, ili kuzuia vurugu zinazoweza kuepukika.
“Inawezekana kabisa kutoa matokeo siku hiyo hiyo kwa majimbo 54 ya Zanzibar. Naamini kuwa ikifika saa sita za usiku matokeo yote ya Zanzibar yatakuwa yamekamilika, hivyo Tume wajitahidi wayatangaze ili wananchi wapate kutulia,” alieleza.
Maalim Seif amesisitiza haja ya kuwepo kwa uchaguzi wa amani, na kuwata vijana wa chama hicho wasikubali kuchokozeka na kupelekea kuvunjika kwa amani ambayo ni hazina kubwa kwa taifa.
Kuhusu Masheikh wa Jumuiya ya Uamsho wanaoshikiliwa Tanzania Bara, Maalim Seif amesema siku zao za kukaa ndani sasa zinahesabika kwani iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar atawarejesha masheikh hao Zanzibar ndani ya kipindi cha wiki moja baada ya kuapishwa.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema iwapo Maalim Seif atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, atayarejesha yale yote yaliyoahidiwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za elimu na afya bila ya malipo.
Mjumbe wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Janeth Fussi, akizungumza katika mkutano huo amesema Maalim Seif anatosha na anavyo vigezo vyote vya kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar.
Katika mkutano huo jumla ya vijana 39 wa jimbo la Mkwajuni kutoka CCM walijiunga na CUF na kukabidhiwa rasmi kadi za chama hicho baada ya kumkabidhi mgombea huyo wa Urais kadi zao.

No comments:

Featured Post

Ronaldo kaonyesha yeye ni mwamba dhidi ya Salah

Mchezaji  wa klabu ya Real Madrid na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno amefunga magoli mawili  (2) katika mechi kati ya Ureno na Misri...