Na Baraka Mbolembole
Wawakili waTanzania Bara katika michuano ya ligi ya mabingwa Afrika, timu ya Yanga SC Jumamosi hii watakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha wanaishinda na kuiondoa Zanaco FC ya Zambia na kufuzu kwa hatua ya makundi kwa mara ya pili katika ligi ya mabingwa Afrika.
Timu hizo mbili zilifungana 1-1 wiki iliyopita katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam hivyo Yanga inahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ya kuanzia mabao 2-2. Nimeona nikuletee orodha yote ya michezo ya mtoano ambayo Yanga imecheza katika michuano ya Caf katika kipindi hiki cha miaka 10.
2007
APRIL 6, 2007 ikicheza ugenini Tunis dhidi ya Esperance katikamchezo wa kwanza hatua ya pili klabu bingwa Afrika,Yanga SC ilikutana na kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Esperance ya Tunisia . katika mchezo wa marejeano Dar es Salaam, Watunisia hao walilazimisha suluhu-tasa na kuwaondoa mashindanoni mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania Bara kwa jumla ya magoli 3-0 baada ya dakika 180.
Baada ya kuondolewa katika ligi ya mabingwa Yanga iliangukia katika michuano ya kombe la Shirikisho na huko wakakutana na El Merreikh ya Sudan. Mchezo wa kwanza jijini Mwanza ulimalizika kwa suluhu-tasa na waliporudiana jijini Kharthoon, Yanga ilichapwa 2-0 na kuondolewa katika michuano hiyo kwa jumla ya mabao 2-0 baada ya dakika 180 za mipambano miwili.
2009
Januari 31 ikicheza nyumbani dhidi ya Wacomoro, Etoile d’Or Mirontsy wawakilishi wa Tanzania Bara, Yanga ilichomoza na ushindi wa mabao 8-1. Wiki mbili baadae wakashinda 6-0 ugenini na kusonga mbele katika michuano ya mabingwa Afrika kwa Jumla ya mabao 14-1 baada ya dakika 180 za mipambano hiyo miwili.
Baada ya kuvuka hatua hiyo ya awali, Yanga ilikutana na mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo Al Ahly ya Misri na kuchapwa 3-0 jijini Cairo, hii ilikuwa Machi 16 na waliporudiana katika mchezo wa Dar es Salaam, Yanga wakalambwa tena safari hii wakichapwa 1-0 na kuondolewa katika michuano kwa jumla ya mabao 4-0 baada ya michezo miwili baina yao kumalizika.
2011
Januari 29, 2011 inabaki kuwa siku mbaya zaidi kwa mashabiki wa Yanga kwani walishuhudia timu yao ikiruhusu mabao manne katika uwanja wa Taifa dhidi ya Wahabesh, Dedebit FC hadi mapumziko wenyeji walikuwa nyuma kwa mabao 3-1. Dakika 90 zilimalizika kwa sare ya 4-4 na mchezo huo unabaki katika historia kwa maana Yanga iliruhusu magoli mengi kuliko ikicheza nyumbani.
Wikimbili baadae walienda Adis Ababa wakiwa na matumaini finyu ya kusonga mbele na wakakutana na kipigo cha 2-0 hivyo kuondolewa katika michuano kwa jumla ya mabao 6-4 baada ya dakika 180.
2012
Machi 3, 2012 Yanga ilirejea tena katika michuano ya ligi ya mabingwa na safari hii walianza kwa sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Zamalek ya Misri. Walipokwenda Cairo mambo yakawa magumu kwa mara nyingine na wakachezea 1-0 hivyo kuondolewa katika hatua ya kwanza tu kwa jumla ya mabao 2-1.
2014
Februari 8, 2014 Yanga iliendeleza umwamba wake dhidi ya timu kutoka Comoro baada ya kushinda 7-0 dhidi Komorozine katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Wakashinda tena 5-2 ugenini na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 12-2.
Machi 1, wakafanikiwa kupata ushindi wao wa kwanza dhidi ya Al Ahly ya Misri katika uwanja wa Taifa baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0. Waarabu hao wakashinda Cairo 1-0 na hivyo mchezo huo wa raundi ya kwanza ukaamuliwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalty kufuatia dakika 180 kumalizika kwa sare ya 1-1. Yanga ikaondolewa kwa jumla ya penalty 4-3 na kuaga michuano.
2015
Februari 14, ikicheza nyumbani dhidi ya Wabotswana, BDF XI , Yanga ilifanikiwa kushinda 2-0 katika mchezo wa raundi ya kwanza wa michuano ya Confederation Cup. Wakachapwa 2-1 ugenini lakini walifanikiwa kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2.
Baada ya kuwaondoa Wabotswana hao, Yanga ilikutana na FC Platnum kutoka Zimbabwe. April 4 wakicheza uwanja wa Taifa Dar es Salaam,Yanga ilifanikiwa kushinda 5-1. Wakachapwa 1-0 ugenini lakini wakafanikiwa kusonga mbele kwa jumla ya mabao 5-2.
April 18 wakicheza nyumbani dhidi ya Etoile du Saleh ya Tunisia, Yanga ililazimishwa sare ya kufungana 1-1 katika mchezo wa kwanza kuamua timuitakayofuzu kwa hatua ya makundi. Wiki mbili baadae wakakubali kipigo cha 1-0 ugenini na kuondolewa katika michuano kwa jumla ya mabao 2-1.
2016
Yanga walirejea katika ligi ya mabingwa na safari hii walianzia ugenini dhidi ya Cercle de Joachim kutoka Mauritius februari 13 walishinda 1-0 ugenini , wakashinda tena 2-0 jijini Dar es Salaam na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-0 baada ya kukamilika kwa dakika 180.
Wakakutana na APR kutoka Rwanda katika raundi ya kwanza na kushinda 2-1 jijini Kigali. Waliporudiana Dar es Salaam, Yanga ililazimishwa sare ya kufungana 1-1 na wakafanikiwa kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2.
Kwa mara nyingine wakakutana na Al Ahly ya Misri . mchezo wa kwanza nyumbani Yanga ililazimishwa sare ya kufungana 1-1 ,katika mchezo wa marejeano wakachapwa 2-1 na kuondolewa katika ligi ya mabingwa kwa jumla ya mabao 3-2. Wakaangukia katika ‘play off’ ya Caf Confederation Cup.
Mei 7, wakicheza nyumbani walianza vyema michuano hiyo kwa kuichapa Esperanca ya Angola kwa mabao 2-0. Wakapoteza ugenini 1-0 lakini walifanikiwa kusonga mbele na kufuzu kwa hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika michuano ya Confederation.
2017
Februari 12 ikicheza ugenini dhidi ya Ngaya Club kutoka Comoro, Yanga ilifanikiwa kushinda 5-1 katika mchezo wa kwanza wa ligi ya mabingwa. Wakalazimishwa sare ya kufungana 1-1 nyumbani katika mchezo wa marejeano na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 6-2.
Machi 11, wakalazimishwa sare ya kufungana 1-1 na Zanaco kutoka Zambia na timu hizo zitarudiana Jumamosi hii na mshindi wa jumla katika mipambano hiyo miwili atafuzu kwa makundi ligi ya mabingwa msimu huu. Kila la heri Yanga SC.
No comments:
Post a Comment