Thursday, 14 December 2017

ajinyonga kisa kukataliwa na mpenzi wake

Ajinyonga Kisa Kukataliwa na Mpenziwe
MKAZI wa kitongoji cha Ndondobya katika kijiji cha Fubu, Kyela mkoani Mbeya, Labson George (22), amejiua kwa kujinyonga na mtandio kwa madai kuwa mwanamke aliyekuwa mpenzi wake wa muda mrefu kukataa kuoana naye.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Abdul Mwamafupa, alisema kijana huyo alikuwa na uhusiano wa muda mrefu na Violet Joseph na inadaiwa kuwa alipomfuata na kupanga kumweleza kuwa waoane, alikataa.

Kutokana na hatua hiyo, alisema George alimnyang’anya mtandio na kutokomea kusikojulikana hadi alipokutwa saa 10:00 jioni pembezoni mwa Mto Mbaka akining’inia juu ya mti akiwa amejinyonga.

Baada ya tukio hilo, alisema serikali ya kijiji ilitoa taarifa polisi ambao walifika wakiwa na daktari na kumtoa kwenye mti aliokuwa amejinyonga.

Mwamafupa alisema kumekuwapo na uvumi mitaani kuwa chanzo cha kijana huyo kujiua ni kutokana na kumfumania mpenzi wake akifanya ngono na mwanamume mwingine vichakani.

Hata hivyo, alisema habari hizo si za kweli bali alijinyonga baada ya mpenzi huyo kukataa kuoana naye akimhisi kijana ana michepuko mingi.

“Kijana huyu kabla umauti haujamkuta aliandika meseji kwa dada yake anayeishi Iringa kuwa ‘Dada yule mwanamke Violet niliyepanga kuoana naye amenikataa ghafla, naamua kujiua ili nisiwepo tena duniani maana amekula pesa zangu nyingi, nahisi amepata wengine’’, alisema.

Alisema baada ya kumtoa kwenye mti walikagua mfukoni na kukuta barua ikiwa na ujumbe kuwa ameamua kujiua kwa sababu mwanamke amekataa kuolewa naye wakati amekula pesa zake nyingi, hivyo hakuona sababu ya kuendelea kuishi duniani kuendelea kuwa na machungu.

Akizungumzia tukio hilo, Violet aliyekuwa mpenzi wa Joseph, alisema chanzo cha kukataa kuoana naye ni kwamba alikuwa na wanawake wengi kutokana na umaarufu alio nao wa kucheza mpira wa mchangani, hivyo alihofia kupata magonjwa  na kufa na kumuacha mama yake ambaye ni mlemavu bila msaada.

Joseph Mwambunga, baba mzazi wa msichana huyo, alimweleza mwandishi wa habari hii kwamba kijana huyo alikuwa na uhusiano wa muda mrefu na binti yake na aliwahi kumfuata na kumweleza kuwa amuoe aache kumchezea na baada ya hapo akashangaa siku iliyofuata amejinyonga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, licha ya kukiri kuwapo  tukio hilo, alitoa rai kwa wananchi kuacha kuchukua uamuzi mgumu wa aina hiyo na kusema kama mtu mpenzi amemkataa, anapaswa kuvuta subira na kutafuta namna ya kumbembeleza, lakini si kujiua.

Mwili wa kijana huyo ulizikwa jana kijijini hapo baada ya vipimo vya kitabibu na uchunguzi wa kipolisi kukamilika hivyo kubainika kuwa alijinyonga kwa mtandio

No comments:

Featured Post

Ronaldo kaonyesha yeye ni mwamba dhidi ya Salah

Mchezaji  wa klabu ya Real Madrid na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno amefunga magoli mawili  (2) katika mechi kati ya Ureno na Misri...